Monday , 9th May , 2016

Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania Serengeti Boys kimetakiwa kuondoa wasiwasi kwa timu watakazokutana nazo katika mashindano maalumu ya soka ya Kimataifa kwa vijana yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini India (AIFF).

Mwenyekiti wa Baraza la Micheo nchini (BMT) Dioniz Malinzi amesema, timu wanazokutana nazo vijana hao ni za kawaida hivyo wanatakiwa kucheza soka ambalo litaipa timu ushindi katika mashindano hayo.

Malinzi amesema, anaamini vijana hao wataweza kufika mbali zaidi katika soka iwapo watazingatia yale waliyofundishwa na walimu.

Kwa upande wake Nahodha wa Serengeti Boys, Issa Abdia amesema, wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano hayo ambayo Tanzania itafungua dimba na Marekani na wanaamini watafanya vizuri katika mashindano hayo na watarudi na kombe.

Ratiba ya michuano inaonyesha kwamba Tanzania itafungua dimba na Marekani kwenye Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa huku mchezo wa pili ukiwa kati ya wenyeji India dhidi ya Malysia Mei 15, mwaka huu.

Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 17, kucheza na wenyeji India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti Boys watacheza dhidi ya Korea Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza dhidi ya Malysia Mei 21.Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali, utachezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa.

Kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo maalumu ya vijana Kimataifa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi cha Serengeti Boys, kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za vijana barani Afrika dhidi ya Shelisheli Juni 25 hadi Julai 2 mwaka huu.