Thursday , 17th Jul , 2014

Kocha Serengeti Boys asema “Tunaiheshimu Afrika Kusini, lakini hatuiogopi. Morali ya wachezaji ipo juu na wanajiamini. Kimsingi wanajua kuwa hii ndiyo njia ya wao kutokea kwenye mpira wa miguu, kwa hiyo lengo ni kushinda mchezo wa kesho,”

Kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Tanzania wenye umri chini ya miaka 17 Serengeti Boys.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Hababuu Ali Omari amesema morali ya wachezaji wake ipo juu kwa ajili ya mechi dhidi ya Afrika Kusini (Amajimbos) itakayochezwa hapo kesho

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 itafanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni

Akizungumza na East Afrika Radio na TV hii leo kwenye kambi ya timu ya Serengeti Boys zilizopo katika hostel za shirikisho la soka nchini TFF jijini Dar es Salaam maeneo ya karume kocha Hababuu amesema nia ya kikosi chake ni kuhakikisha wanafika kwenye fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Niger

Naye nahodha wa kikosi hicho Omar Waine amesema wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi hapo kesho na hivyo amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi ili kuwaunga mkono katika kutimiza azma hiyo.