Tuesday , 18th Dec , 2018

Klabu ya soka ya KMC kupitia kwa kocha wake Ettiene Ndayiragije, imesema imejiandaa vyema na mchezo wake wa kesho dhidi ya Simba kwani mchezo huo ni sehemu ya ratiba japo ni kipimo kwa wachezaji wake.

Wachezaji wa Simba wakifanya mazoezi

Ndayiragije raia wa Burundi, ameweka wazi kuwa ukubwa wa Simba tu ndio unafanya mchezo huo uwe na tofauti lakini walitambua watacheza na Simba kwasababu wote wapo ligi kuu.

"Vijana wapo vizuri na Simba Sc ni timu nzuri yenye ushindani na inawakilisha nchi kwahiyo ni kipimo kizuri kwa KMC kujua maendeleo ya kikosi chetu," amesema Ettiene Ndayiragije.

KMC ambayo ipo katika nafasi ya 9 ikiwa na alama 21 baada ya mechi 16, inakuatana na Simba kwenye mchezo wa ligi kuu utakaopigwa kwenye uwanja wa taifa Dar es salaam.

Simba ambayo imerejea kutoka nchini Zambia, ilipokuwa inacheza mchezo wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Nkana Red Devils na kufungwa 2-1, ipo katika nafasi ya 3 ikiwa na alama 27 kwenye michezo 12.