Friday , 19th Jan , 2018

Mkurugenzi wa timu ya Singida United, Festo Sanga amefunguka na kudai kilichopelekea kufungwa kwa klabu yake mabao 4-0 dhidi ya Simba siku ya jana (Alhamisi) ni kutokana na mapungufu yaliyokuwepo kwa walinzi wa timu hiyo.

Festo ameeleza hayo ikiwa imepita siku moja tokea ulipochezwa mpambano huo katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaama, katika mzunguko wa 13 Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inaendelea kutimua vumbi.

"Mchezo tuliocheza jana dhidi ya Simba umetusikitisha sana, kwa kuwa hatukutegemea matokeo ya namna ile lakini tunawapongeza Simba kwa sababu jana walikuwa bora kuliko sisi na walionyesha mpira wa hali ya juu", alisema Festo.

Pamoja na hayo Festo ameendelea kwa kusema "kwa kweli mabeki wetu walikuwa na mapungufu makubwa na kupelekea kufungwa mabao 4. Ni kitu cha kwanza tangu tucheze Ligi Kuu Tanzania Bara kuruhusu kufungwa mabao zaidi ya 2 katika mchezo. Ila naweza kusema tumepoteza mchezo na wala hatujapoteza mapambano", alisisitiza Festo.

Timu ya Singida United kwa sasa inashikilia nafasi ya nne ikiwa na alama 23 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku nafasi ya tatu ikishirikiwa na Mtibwa Sugar kwa alama 24, Azam FC wakiwa nafasi ya pili kwa alama 27 huku Simba SC wakiwa kidedea kwa alama 29.