Saturday , 3rd Jun , 2017

Michuano ya mpira wa kikapu ya 'Sprite BBALL KINGS' iliyorindima leo kwenye viwanja vya JK Park, jijini  Dar es salaam imeacha gumzo kwa wapenzi wa mchezo huo waliojitokeza na kusema hawajawahi kuona mashindano yenye upinzani mkali kama hayo.

UDSM walipotwaa point 42 kwa 5 dhidi ya Dandy

Michuano hii imezikutanisha timu 42 kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kucheza mchezo wa kwanza wa kufuzu kuingia kwenye timu 16 bora ambazo zitaingia kwenye hatua ya mtoano. 

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya michuano hiyo, Kamishna wa ufundi na Uendeshaji mashindano wa Shirikisho la mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Manasseh Zablon amesema timu zilizoweza kufuzu hatua ya 16 bora wanapaswa kujipanga kikamilifu katika kuelekea mchezo wa mtoano, ambapo siku ya Jumatatu inatarajiwa kuendeshwa droo ya wazi ambayo itapanga ratiba nzima za mchezo utakavyokuwa unaendelea. 

"Timu zilizofuzu katika hatua hii, zitaingia moja kwa moja kwenye hatua ya 16 bora hivyo nawaomba mtoe mwakilishi wenu mmoja kutoka kila timu ili aweze kuja kushuhudia droo ya wazi ya kupanga ratiba za mechi za hatua ya mtoano siku ya Jumatatu" alisema Zablon akiziambia timu zilizofuzu leo hii.

Kamishna wa ufundi na Uendeshaji mashindano wa Shirikisho la mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Manasseh Zablon

Timu zilizofanikiwa kuingia 16 bora na pointi ilizopata; DMI pointi 58, Dream Cheaser pointi 52,UDSM pointi 37, Oysterybay pointi 37, Ukonga Warriors pointi 25, The fighter pointi 22 huku timu zilizopata ushindi bila ya wapinzani wao kuingia uwanjani na kupewa pointi 20 za bure ni Bongo hits, Chanika Legends, The force one , Lous Montfort, Heroes B, Makongo Juu, TMT, Mchenga, Kurasini Heat pamoja na Land Force.

Pamoja na hayo, timu zilizotakiwa kushiriki katika michuano hii zilipaswa kuwa 52 lakini timu 10 zilishindwa kuwepo uwanjani bila taarifa.

Baadhi ya mashabiki waliokuwepo Kidongo chekundu.