Tuesday , 13th Nov , 2018

Tanzania huenda ikawa na nafasi nzuri ya kuweka historia endapo timu zake mbili za taifa (Taifa Stars na Ngorongoro Heroes), zitafuzu katika mashindano ya AFCON ambapo tayari timu 2 zingine zimeshafuzu kushiriki.

Juu kushoto ni Taifa Stars, Chini Serengeti Boys na Ngorongoro Heroes.

Timu ya vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), tayari imeshafuzu kupitia tiketi ya kuwa wenyeji wa michuano hiyo itakayofanyika kuanzia April 14 hadi 28, 2019 hapa nchini.

Timu nyingine ambayo imeshafuzu AFCON ni timu ya taifa ya soka la Ufukweni ambayo itashiriki michuano hiyo itakayofanyika Desemba 8 hadi 14 mwaka huu nchini Misiri.

Timu ya tatu ya Tanzania ambayo inawania kufuzu AFCON 2019 ni ya vijana chini ya miaka 23, (Ngorongoro Heroes) ambayo imeondoka leo asubuhi kuelekea Burundi ambapo kesho itacheza na Burundi katika mchezo wa kutafuta tiketi ya kufuzu AFCON.

Timu ya 4 ni Taifa Stars ambayo inawania kufuzu AFCON 2019, na Novemba 18, 2018 itakuwa uwanjani ugenini kucheza na Lesotho kwenye mchezo wa kundi L ambapo Stars ina alama 5 nyuma ya Uganda yenye alama 10.

Hii ni nafasi ya pekee kwa Tanzania kuweka historia endapo itafuzu kucheza fainali hizo ambazo ni michuano mikubwa zaidi barani Afrika kwa timu zote za taifa.