Friday , 19th Jan , 2018

Klabu ya soka ya Simba kupitia kamati yake ya utendaji chini ya Kaimu Rais Salim Abdallah imeteua kamati ya nidhamu ambayo itasimamia nidhamu za wachezaji.

Akitangaza kamati hiyo leo mkuu wa idara ya habari ya klabu hiyo Haji Sunday Manara amesema kamati hiyo imeundwa mahsusi kusimamia nidhamu ndani ya klabu hiyo hasa nidhamu za wachezaji.

''Kamati ya utendaji imeteua kamati mbili, kamati ya nidhamu na kamati ya maadili, kamati ya nidhamu hasa hasa itasimamia masuala ya nidhamu za wachezaji na kamati zote zitafanya kazi kwa mujibu wa katiba ya Simba'', amesema Manara.

Aidha Manara amemtaja Mwenyekiti wa kamati hiyo kuwa ni Aziz Kifile huku wajumbe wakiwa ni Alhaj Hassan Mnyinye, Malota Soma, David Mihambo na Egbert Muhaga.

Pia Simba imetumia mkutano huo wa leo na wanahabari kumtambulisha kocha mpya Pierre Lechantre ambaye pia amesaini mkataba ambao haujawekwa wazi ni wa muda gani.