
Haji Manara (kushoto), Dismas Ten (katikati), Masau Bwire (kulia)
Katika uchambuzi huu, tunakuletea listi ya wasemaji tano bora wa vilabu vya Ligi Kuu Tanzania Bara katika mwaka 2018.
Haji Manara (Simba SC)
Haji Sunday Manara ni Afisa Habari mbaye amejizolea umaarufu mkubwa katika mwaka 2018 hasa kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram. Amekuwa akihusika katika kila tukio kubwa linaloihusu Simba, liwe la nje au ndani ya uwanja, pia mejizolea umaarufu katika utani dhidi ya mahasimu wao Yanga, ambapo mara kwa mara amekuwa aki'post' picha mbalimbali zenye maneno yenye utani kwa hasimu wake, jambo ambalo limekuwa likiongeza umaarufu wake.
Masau Bwire (Ruvu Shooting)
Masau Bwire ameendelea kujizolea umaarufu katika soka nchini Tanzania hasa pale alipokuwa akihojiwa juu ya timu yake ya Ruvu Shooting. Ameibua misemo maarufu katika soka mwaka huu kama 'Mpapaso' ambao unaelezea namna ambavyo amekuwa akijigamba juu ya timu yake kupata matokeo.
Dismas Ten (Yanga SC)
Afisa Habari huyu wa vinara wa Ligi Kuu hivi sasa, ameibuka na kupata umaarufu mkubwa mwaka 2018 hasa baada ya kuanza kuweka picha mbalimbali katika mitandao ya kijamii zinazoonesha kujibu mapigo kutoka kwa hasimu wake Haji Manara wa Simba. Pia amekuwa thabiti katika kusimamia kitengo cha habari ndani ya klabu hiyo ikiwemo kuiendeleza Yanga Tv.
Jaffar Idd (Azam FC)
Jaffar Idd Maganga ameendelea kuwa imara katika kuisemea Azam FC na kuhakikisha klabu hiyo inakuwa kubwa katika mwaka 2018. Sifa yake kubwa amekuwa hajihusishi na masuala ya utani binafsi na vilabu vingine kutokana na kutokuwa na akaunti maarufu katika mitandao ya kijamii.
Amekuwa thabiti katika kuhabarisha vitu muhimu vya klabu yake pamoja na kuhakikisha Azam inapewa heshima, mfano mzuri ni hivi karibuni wakati Azam FC ilipokuwa ikiongoza ligi alipolalamika kuwa vyombo vya habari haviipi heshima inayostahili klabu hiyo.
Clement Sanga (Lipuli FC)
Kwa wadau wengi wa soka, huyu ni mtu anayefahamika kutokana na kuwa thabiti katika kutoa taarifa mbalimbali za klabu ya Lipuli. Licha ya uchanga wa klabu yake katika ligi kuu, ameweza kuisimamisha vizuri Lipuli FC katika mitandao ya kijamii, ambapo amekuwa akitoa taarifa mbalimbali katika ukurasa maalum wa klabu na hata yeye mwenyewe mara kwa mara kuzungumza na wanahabari juu ya maendeleo ya klabu yake.