Tuesday , 3rd Mar , 2015

Klabu ya Yanga imesema, kutokana na Bodi ya Ligi kuu Tanzania bara kubadilisha ratiba bila kuwapa taarifa mapema, hawatacheza mechi hiyo dhidi ya JKT Ruvu ambayo badala ya kuchezwa hapo kesho itachezwa Machi 11 mwaka huu jijini Dar es salaam.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Afisa habari wa Yanga, Jerry Muro amesema, kitendo cha kubadilishiwa ratiba inaonekana wazi ni kutaka kuwakomoa kwani Machi 14 wanamechi ya Kombe la shirikisho mzunguko wa pili dhidi ya Fc ya nchini Zimbabwe hivyo wanatakiwa kufanya maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo..

Muro amesema,maamuzi yaliyochukuliwa na bodi ya ligi ni kama kuwakomoa na kuangalia mechi hiyo ya kombe la shirikisho kuwa ni ya klabu pekee na sio ya Tanzania ambao ni washiriki pekee waliobakia katika michuano hiyo.

Kwa upande mwingine Muro amesema, mabadiliko ya sheria yaliyowekwa dhidi ya vilabu shiriki vya Ligi kuu soka Tanzania Bara ya mchezaji anapopata kadi tatu za njano na kuchagua mechi nipi acheze na ipi asicheze sio sahihi.

Muro amesema, Bodi ya Ligi imefanya kosa kukubali ombi la mchezaji wa Simba Ibrahim Ajibu ambaye alikuwa na kadi tatu za njano na kuomba acheze mechi ya Simba dhidi ya Tanzania Prisons iliyochezwa Februari 28 pamoja na mechi ya Simba dhidi ya Yanga itakayochezwa Machi nane mwaka huu.

Muro amesema, vitendo hivyo vinaonyesha wazi ni jinsi gani viongozi wa Bodi ya Ligi wasivyokuwa makini kwa ajili ya kupanga taratibu za soka hivyo kupelekea Tanzania kila mara kuonekana kichwa cha mwendawazimu kwa upande wa michezo hususani soka.