Beki wa yanga hajji mwinyi kulia(picha)akijaribu kumpita wa Simba Ramadhani Kessy .
Mabao ya Yanga yaliyopeleka msiba mitaa ya Msimbazi jioni ya leo yamewekwa kambani na washambuliaji wa kimataifa Donald Ngoma dakika ya 39 kufuatia na makosa ya beki Hassan Kessy na la pili likisukumiziwa kimiani na mrundi Amisi Tambwe aliyemalizia krosi ya Geofrey Mwashiuya mnamo dakika ya 72.
Maafa kwa Simba yalianza mnamo dakika 25 kufuatia nyota wa klabu hiyo Abdi Banda kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu na mwamuzi Jonesia Rukyaa kufuatia kumfanyia madhambi mshambuliaji wa Yanga Donald Ngoma.
Licha ya kupoteza mechi hiyo Simba ilijaribu kujitutumua na kupata kona nane kwenye mechi hiyo huku Yanga ikipata kona moja pekee.
Kwa matokeo hayo wanajangwani wanarejea kileleni mwa ligi hiyo wakifikisha pointi 46 huku Simba ikiporomoka mpaka nafasi ya tatu kwa pointi zao 45 na hii ni kutokana na matokeo ya Azam FC ambayo hii leo imekwea mpaka nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 45 baada ya kuinyuka Mbeya City kwa jumla ya mabao 3-0.
Mabao ya Azam yamewekwa kimiani na washambuliaji Kipre Tchetche, John Bocco na Farid musaa.
Matokeo ya mechi zilizopigwa kwenye viwanja vingine hapa nchini Mgambo JKT na Tanzania Prisons wamefungana bao 1-1 kwenye mechi iliyopigwa katika uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Stand United ikiwa nyumbani Kambarage mjini Shinyanga ikatoka sare ya bao 1-1 na JKT Ruvu nayo Toto Africans wakatoka sare tasa na Kagera Sugar.
Kesho Majimaji itaikaribisha Mtibwa Sugar katika uwanja wa Majimaji mjini Songea,Mwadui itaumana na Coastal Union ya Tanga nayo Ndanda FC Itaialika African Sports katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.