Friday , 14th Oct , 2016

Serikali ya Mkoa wa Simiyu imesema kuwa imejipanga kuitosheleza nchi kwa bidhaa mbalimbali zitakazotengenezwa mkoani humo kupitia viwanda vitakavyoanzishwa ambavyo vitatumia zaidi malighafi za ndani ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka.

Akizungumza Mkoani humo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amesema kuwa serikali yake ya mkoa imedhamiri kuondoa aibu ya nchi ya kuagiza vitu ambavyo nchi inaweza kutengeneza kwa kuwa kuna malighafi nyingi za kuweza kuanzisha viwanda nchini.

Mtaka amesema kwa kuanza mkoa wake umeanza kutengeneza chaki zake wenyewe ili kuitosheleza sekta ya elimu mkoani humo lakini pia wamedhamiria kuishibisha nchi kwa kutengeneza vifaa katika sekta ya afya kwa kutumia pamba inayolimwa katika kanda hiyo.

Aidha Mhe. Mtaka ameongeza kuwa kauli mbiu ya mkoa huo ni 'Bidhaa Moja Wilaya Moja' ikiwa na lengo la kila wilaya iweze kuanzisha kiwanda ambacho kinaweza kutengeneza bidhaa ambao itaweza kuwasaidia wananchi na kukuza uchumi wa mkoa pamoja na nchi kwa ujumla.

Ameongeza kuwa kupitia makongamano, wajasiriamali kwa vijana na wanawake mkoani humo wameweza kujifunza utengenezaji wa bidhaa tofauti hivyo anatarajia mkoa huo kuwa wa kwanza katika utekelezaji wa sera ya ukuaji wa uchumi kupitia viwanda.