Monday , 26th Feb , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza kamanda wa  (TAKUKURU) mkoa wa Mtwara Bw. Stephen Mafipa kumtafuta popote alipo na kumkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi Bw. Fortunatus Kagoro kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na watumishi na Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Masasi na Halmashauri ya wilaya ya Masasi akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara na kuagiza pia kukamatwa kwa Kaimu Mweka Hazina Bw. Heri Hamad pamoja na  Afisa Mipango Bi Teresia Nsumba.

"Lazima fedha za serikali zitumike kama ilivyokusudiwa na baada ya uchunguzi kukamilika watakaobainika kwamba wahajahusika na ubadhilifu huo watarudishwa kazini", amesema Waziri Majaliwa.

Watendaji hao wanadaiwa kutumia sh. bilioni 1.8 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Mji wa Masasi kwa kuchora mchoro na kujenga msingi katika maeneo mawili tofauti.

Waziri Mkuu amesema  mwaka 2014  serikali ilipeleka shilingi milioni 575 wilaya Masasi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la halmashauri hiyo na fedha hizo ziliishia kutumika  katika hatua za maandalizi ya awali ikiwa ni pamoja na kutengeneza michoro ya jengo na ilipofika mwaka 2016/2017 serikali ilipeleka tena sh. bilioni 1.25 kwa ajili ya ujenzi huo, ambapo halmashauri hiyo ilienda kutafuta eneo lingine na kufanya tena shughuli zilizokuwa zimefanyika na kuanza ujenzi ambao umeishia katika msingi na fedha zimeisha.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka watendaji hao kutotumia fedha za makusanyo ya ndani kwa ajili ya kuziba pengo la fedha za mradi huo ambazo baadhi yake hazijulikani zilipo na amewaagiza Madiwani kutoruhusu jambo hilo. 

"Madiwani msikubali kutumia fedha za makusanyo ya ndani kupeleka kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo ambayo tayari Serikali ilishatoa fedha ya ujenzi wake", amesisitiza Waziri Majaliwa.

Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali inahitaji kuona fedha za maendeleo zinazopelekwa katika halmashauri mbalimbali nchini zinatumika kama ilivyoelekeza na si vinginevyo na serikai haitakuwa na mzaha kwa mtumishi atakayezitumia vibaya.