
Waziri wa kilimo Mh. Japhet Hasunga.
Hayo yamebainishwa tarehe 24 Novemba 2018 na Waziri wa kilimo Mh. Japhet Hasunga, wakati akizungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Mbegu (ASA) katika ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mh. Rais Dkt John Pombe Magufuli imejipambanua katika usimamizi madhubuti wa ujenzi wa viwanda hivyo wananchi wanapaswa kuzalisha kwa wingi mazao mbalimbali katika sekta ya kilimo kwani uhai wa viwanda vingi vinategemea zaidi sekta ya kilimo.
Alisema kuwa Wizara ya kilimo itasimamia kwa weledi uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu bora na kwa wingi ili wakulima waweze kunufaika katika uzalishaji wenye tija ili kuondokana na uzalishaji wa mazao kwa ajili ya chakula pekee badala yake kuzalisha kwa tija kilimo cha kibiashara.
“Katika viwanda tutakavyozalisha zaidi ya asilimia 60 ya malighafi zitakazotumika zinazalishwa hapa nchini, hivyo tunawajibu wa kutoa malighafi zinazotosheleza viwanda tunavyovianzisha” Alikaririwa Mh Hasunga.