Monday , 26th Nov , 2018

Kuelekea mchezo wa klabu bingwa Afrika kati ya Simba SC dhidi ya Mbabane Swallows utakaopigwa Jumatano, Novemba 28 jijini Dar es salaam, klabu ya Simba imemuomba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo, awe mgeni rasmi.

Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo na Msemaji wa Simba Haji Manara.

Akiongea na waandishi wa habari leo, msemaji wa timu hiyo Haji Manara, amesema maandalizi yote yamekamilika wanasubiri tu jibu la Mh. Jafo kama atakuwa na nafasi ya kuhudhuria.

''Tumerejea kimataifa na Jumatano tunaanza rasmi safari hiyo ngumu na ndefu ambapo tunaanza na Mbabane Swallows na tunatarajia mechi hii mgeni rasmi atakuwa mbunge wa Kisarawe Selemani Jafo'', amesema.

Amesema kwa upande wa timu, ipo kambini na wachezaji wote wako fiti wanaendelea na maandalizi isipokuwa mlinzi wa kulia Shomari Kapombe ambaye ni majeruhi na tayari ameshafanyiwa upasuaji huko Afrika Kusini.

Aidha Manara amefafanua kuwa wachezaji wa kimataifa kutoka Uganda Emmanuel Okwi na Juuko Murshid wanarejea leo nchini kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa na watajiunga na kambi moja kwa moja.

Kuhusu wapinzani wao, Manara amesema wanawasili leo jijini Dar es salaam saa 7:00 usiku tayari kwa mchezo huo utakaopigwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.