Monday , 26th Nov , 2018

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua huduma za viza na vibali vya ukaazi vya kielektroniki na kuwataka watu wote watakaopewa vibali hivyo kutii sheria kwa kufanya shughuli ambazo wameelekezwa kwa mujibu wa vibali vyao na si vinginevyo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Amesema utoaji wa huduma hizo ni miongoni mwa jitihada za Serikali katika kuvutia uwekezaji, hususani katika sekta ya viwanda kwani hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa vibali hivyo kwa raia wa kigeni na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba 26, 2028) wakati akizindua huduma za viza na vibali vya ukaazi vya kielektroniki katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kwamba hatua hiyo itasaidia kuondoa urasimu na ucheleweshwaji wa huduma pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.

Amesema Idara ya Uhamiaji inatarajia kuanza kutoa huduma tajwa kwa raia wa kigeni muda wowote kuanzia sasa na kwa kupitia huduma hiyo, raia wa kigeni wataweza kuomba vibali hivyo kwa njia ya kielektroniki wakati wowote na mahali popote walipo.

Waziri Mkuu amesema watakaopewa vibali wanatakiwa kufanya shughuli zao kwa mujibu wa vibali vyao kwa sababu kufanya shughuli tofauti na ilivyoainishwa kwenye kibali ni kosa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Uhamiaji.

Natoa wito kwa Maafisa, Askari pamoja na Watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji kuhakikisha kuwa mifumo hiyo inatunzwa pamoja na kuendeleza miundombinu yote ya kiutendaji.”