Tuesday , 3rd Sep , 2019

Kocha mkuu wa klabu ya Yanga, Mwinyi Zahera amebainisha sababu ya timu yake kutocheza na Mbao FC katika ziara yao ya Jijini Mwanza.

Baadhi ya wachezaji wa Yanga

Ziara hiyo ya Yanga Jijini Mwanza ni ya kujiandaa na mchezo wa hatua ya pili ya mtoano Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zesco ya Zambia, ambapo itacheza michezo kadhaa ya kirafiki kabla ya kurejea Dar es Salaam, Septemba 11.

Akizungumzia kuhusu ziara hiyo, Zahera amesema kuwa timu yake haitocheza na timu yoyote ya Ligi Kuu kwa kuhofia wachezaji wake wataumizwa bila sababu yoyote ya msingi na kukosa mchezo muhimu mbele yao, hivyo watacheza na timu za kawaida na timu za daraja la kwanza kwa ajili ya mazoezi.

"Siwezi kucheza na Mbao kwa sababu sisi tuna mechi muhimu ya Klabu Bingwa Afrika, wachezaji wetu wanaweza wakakamiwa na wakaumia", amesema.

"Wao hawaoni kama ni mechi ya kirafiki, wao wanakuja na jambo moja tu la kusema kwamba tunataka kumpiga Yanga. Mbao siwakubali kwa sababu wao wanacheza mechi kama vile Klabu Bingwa wakati ni mechi ya kirafiki", ameongeza.

Yanga inatarajia kucheza na Zesco United, Septemba 14 Jijini Dar es Salaam katika mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya pili ya mtoano Klabu Bingwa Afrika, ambapo ilifanikiwa kufika hatua hiyo baada ya kuiondoa Township Rollers kwa jumla ya mabao 2-1 katika hatua ya kwanza ya mtoano.