Wednesday , 4th Sep , 2019

Leo ni siku nyingine ambayo Tanzania itaanza kuandika historia kubwa katika michuano mikubwa kabisa duniani kwa upande wa soka, ikiwa ni hatua ya kufuzu Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Tanzania na Burundi

Timu ya taifa 'Taifa Stars' inaanzia ugenini nchini Burundi ambako hii leo itacheza na wenyeji Intamba mu Rugamba, ambapo katika rekodi za michezo minne ya hivi karibuni timu hizo zimefungana kwa kupata matokeo sawa.

Katika mchezo wa michuano ya CECAFA, Novemba 29 2012, Taifa Stars ilifungwa bao moja na Burundi kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Mchezo mwingine ambao ni wa kirafikiuliozikutanisha timu hizo, Machi 8, 2017, Taifa Stars ilishinda kwa mabao 2-1 katika uwanja wa taifa kabla ya kukutana tena Novemba 14, 2018 kwenye kuwania kufuzu michuano ya AFCON kwa vijana wa U-23, ambapo katika mchezo huo wa awali, Burundi ilishinda kwa mabao 2-0.

Kwenye mchezo wa marudio uliopigwa Jijini Dar es Salaam, Novemba 20, 2018, Taifa Stars ilishinda kwa mabao 3-1 na kufanikiwa kuwaondoa Burundi.

Akizungumza baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege mjini Bunjumbura jana, Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amesema kuwa timu yake iko sawa kuelekea mchezo huo huku akioneshwa kuridhishwa na kiwango cha waandishi wa habari waliojitokeza katika kuwapa hamasa kwa wachezaji ili kufanya vizuri.