Friday , 6th Sep , 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, ameshangazwa na namna Rais wa Uganda Yoweri Museveni,  anavyoendelea kumng'ang'ania Kamishina wa Mamlaka ya Mapato wa nchi hiyo (URA),  ambaye anaonesha kukwamisha ujenzi wa bomba kubwa la Mafuta kutoka Ohima kuja Tanzania.

Rais Magufuli na Rais Museveni

Rais Magufuli ameyabainisha hayo leo Septemba 6 Jijini Dar es Salaam,  wakati wa ufunguzi wa kongamano la kwanza la mwaka kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda, ambapo amemtolea mfano wa namna yeye alivyoweza kuwatumbua makamishina wa TRA takribani watano kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu tangu aingie madarakani.

''Nilikuwa namuuliza Mzee Museveni, mbona unachelewesha hilo bomba kwasababu ya kodi ya huko ambayo umeikataa kuikubali, kodi yenyewe ni dola 600 wakati utakuwa unatengeneza dolla bilioni 80, watu wako wa URA wasikucheleweshe, sisi tulitaka hiyo 'pipeline' iitwe Kaguta, mimi nilipoingia madarakani, simfundishi Mzee, nilibadilisha makamishina watano kwa kipindi cha miaka 3 na nusu, wewe umemng'ang'ania wa nini huko''amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amemshauri Rais Museveni kuhakikisha anaongeza ukali kwa watendaji wake kwakuwa mradi huo utazalisha ajira nyingi na kudai kwamba anatamani ingewezekana awabadilishe watendaji wa Tanzania awapeleke Uganda halafu wa Uganda waje Tanzania awashughulikie japo kwa mwezi moja.