Saturday , 7th Dec , 2019

Baraza la Sanaa la Taifa "BASATA"  limempunguzia adhabu rapa wa kike nchini Tanzania Rosa Ree ya kumfingia miezi 6, na kumruhusu kuendelea na shughuli zake za kisanaa.

Picha ya msanii HipHop Rosa Ree

Barua hiyo  imetoka kwa Katibu Mtendaji wa baraza hilo Godfrey Mngereza  na imeandikwa,

"Baraza la sanaa la Taifa linapenda kukutaarifu kuwa ombi lako la kupunguziwa adhabu limekubaliwa baada ya kujutia kosa lako na kumuandikia barua Mh. Waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo ili kuomba kupunguziwa adhabu", Barua kutoka Basata.

Aidha barua hiyo iliendelea kusema "1. Kuanzia tarehe ya barua hii, unaruhusiwa kuendelea na shughuli za sanaa, hivyo adhabu uliyopewa ya kufungiwa miezi 6  imeondolewa, 2. Kulipa faini ya milioni 2, kama ulivyoagizwa na hii ilipwe ndani ya mwezi mmoja".

Kupitia ukurasa wa mtandao wa Instagram Rosa Ree ameandika "Napenda kutoa shukrani kwa ofisi ya Waziri wa sanaa, habari, utamaduni na  michezo Mhe. Harrison Mwakyembe na BASATA, kwa kuniruhusu kuendelea kufanya shughuli zangu za sanaa, naahidi kufanya kazi zangu ipasavyo na kuendelea kuipeperusha bendera ya nchi yangu"

Ikumbukwe mwezi uliopita Basata walimfungia Rosa Ree kwa muda wa miezi sita na kumtaka alipe faini ya Milioni 2, kwa makosa mawili ambayo ni kuachia video iliyokosa maadili pamoja kufanya kazi nje ya nchi bila kuwa na kibali.