Monday , 9th Dec , 2019

Hatimae Serikali nchini Saudi Arabia, imeruhusu migahawa kuwa na mlango mmoja wa kuhudumia wateja bila kuzingatia jinsia ama familia, ambapo hapo awali ilikuwa lazima kuwa na mlango mmoja kwa ajili ya familia wa wanawake na mwingine wa wanaume.

Namna ambavyo hapo awali kulikuwa kumejengwa ukuta, unaowatenganisha wanawake na wanaume katika migahawa nchini Saudi Arabia.

Sharti hilo kwa sasa limeondolewa, huku migahawa mingi pamoja na maeneo mengine ya kufanyia mikutano ikifuata mkondo huo.

Mapema mwaka huu, agizo kutoka kwa Mfalme lilihitaji wanawake wa Saudia, kuruhusiwa kusafiri hadi Mataifa ya nje bila ya kupata ruhusa ya msimamizi wa kiume, pamoja na kuondoa marufuku ya wanawake kujiendesha wenyewe ambayo ilifikia ukomo wake mwaka 2018, iliyokuwa imedumu kwa miongo kadhaa.

Hata hivyo wanaharakati wanalalamika kwamba, sheria nyingi zinazobagua wanawake bado zinaendelezwa na watu wengi mashuhuri wanaotetea haki za wanawake, wamekamatwa hata wakati ambapo Serikali inafanya mabadiliko haya.

Tangu Mohammed bin Salman alipotawazwa na kuwa Mfalme mwaka 2017, amefanya mabadiliko katika jamii ambayo imekuwa ikikumbatia tamaduni zake za jadi.

Mabadiliko yake yameungwa mkono na jamii ya kimataifa lakini yamekuwa yakikandamizwa.