Tuesday , 17th Dec , 2019

Mrembo wa dunia kwa watu wenye ulemavu wa kusikia kutokea nchini Tanzania Winifrida Brayson, amesema anamshukuru sana Rais John Pombe Magufuli, na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kumpa sapoti na ushirikiano hadi kumfikisha nchini Urusi ambapo mashindano hayo yalifanyika.

Winifrida Brayson

Mrembo huyo ameshinda mataji mawili makubwa duniani yaliyofanyika nchini Urusi, na amekamata nafasi ya kwanza katika  taji la "Miss deaf top fashion model" ambapo kulikuwa na washindani kutoka kwenye nchi 57 tofauti, kisha ameshika nafasi ya 10 katika taji la "Miss Photogenic".

'Naishukuru sana Serikali chini ya Rais Magufuli na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kufanikisha safari yangu ya kwenda Urusi ambako nimeshinda mataji hayo', ameeleza.

Akiendelea na maongezi na EATV & EA Radio Digital mrembo Winifrida Brayson, pia amemtaja mfanyabiashara Mohammed Dewji kama mtu ambaye anatamani kuonana naye,

"Natamani sana kukutana na Mohammed Dewji "Mo" nataka nizungumze naye na shida yangu niliyokuwa nayo nataka nimuelezee yeye kwa sababu nina lengo la kufungua taasisi ya watoto ambao ni wanaulemavu wa kusikia na wanaoishi katika mazingira magumu, pia nataka nimwambie  anisapoti katika masuala ya taasisi " amesema Winifrida Brayson.