Saturday , 11th Jan , 2020

Sultan wa Oman Qaboos bin Said amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Januari 11, 2020. Taarifa ya kifo cha Qaboos imetolewa na TV ya taifa ambapo pia zimetangazwa siku 3 za maombolezo pamoja na siku 40 za bendera kupepea nusu mlingoti. Sultan Qaboos amefariki akiwa na umri wa miaka 79.

Sultan wa Oman Qaboos bin Said

Kupitia EATV & EA Radio Digital, tumekuandalia historia fupi ya maisha ya Sultan Qaboos bin Said na ugonjwa ulioutoa uhai wake.
 
Maisha yake ya awali

Kiongozi Sultan Qaboos bin Said amezaliwa Novemba 18, 1940 na kufariki Januari 10, 2020, amekaa madarakani kwa muda wa  miaka 50, alianza kuiongoza Oman mwaka 1970 hadi umauti unamkuta alikuwa yupo katika uongozi.

Ameweka rekodi ya kukaa madarakani kwa muda mrefu katika nchi za Mashariki ya kati hadi kwenye nchi za falme za kiarabu.

Maisha Binafsi

Sultan Qaboos Bin Said ni mtoto pekee katika uzao wa baba yake ambaye alikuwa kiongozi wa Oman aitwaye Sultan Said bin Taimur na mama yake Sheikha Mazoon al-Mashani, alioa wake watatu katika nyakati tofauti  na katika maisha yake hajawahi kupata mtoto wala ndugu wa kuzaliwa naye tumbo moja.

Elimu

Elimu ya msingi na sekondari alipata katika shule ya Salalah, kisha akahamishiwa shule binafsi ya St Bury St Edmunds nchini Uingereza akiwa na umri wa miaka 16, alivyofikisha miaka 20 alijiunga na chuo cha ufalme wa kijeshi na alipohitimu kozi hiyo mwaka 1962 alijiunga katika jeshi la Uingereza.

Ugonjwa na Kifo

Kuanzia mwaka 2015 alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya Saratani ya utumbo mpana "Colon Cancer", hadi kufikia Disemba 14,2019 kutoka katika hospitali ambayo ilikuwa inampa matibabu UZ Leuven nchini Ubelgiji, ilitangaza kuwa hatachukua muda mrefu wa kuishi duniani, ambapo yeye mwenyewe alitaka arudishwe nyumbani ili umauti ukimfika umkutie akiwa kwao.