Monday , 13th Jan , 2020

Serena Williams miaka 3 bila taji, miaka 38 ya umri, taji la kwanza akiwa mama, ushindi wake autoa msaada.

Serena Williams akiwa na taji lake la WTA Auckland Classic pamoja na familia yake.

Nguli wa mchezo wa tenisi kwa wanawake Serena Williams, amefanikiwa kuchukua taji la michuano ya wazi ya WTA Auckland Classic baada ya jana Januari 12,2020 kushinda fainali kwa seti 6-3, 6-4 dhidi ya Jessica Pegula.

Taji hilo ni la kwanza kwa Serena baada ya miaka mitatu kupita tangu aliposhinda michuano ya wazi ya Australia mwaka 2017.

Pia taji hilo ni kwanza kwa Serena tangu alipopata mtoto wake Alexis Olympia, Septemba 1, 2017.

Serena Williams akiwa na taji lake la WTA Auckland Classic

Na sasa akiwa na umri wa miaka 38, amefikisha mataji 73 yanayotambulika na shirikisho la tenisi kwa wanawake WTA.

Pia amecheza na kushinda mataji ndani ya miongo minne ambapo kwa mara ya kwanza alishinda ubingwa mwaka 1999.

ATOA MSAADA 

Baada ya kushinda ubingwa huo, Serena ametoa kiasi cha $43 000 zaidi ya shilingi milioni 90 kwa wahanga wa janga la moto kule nchini Australia ambapo ndio alichukua ubingwa wake wa mwisho mwaka 2017.