Monday , 27th Jan , 2020

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Hamis Mussa, amesema kuwa hadi sasa yeye pamoja na wenzake watano hawajajua nini hatma yao, kwani bado hawajaitwa kwenye kikao cha nidhamu kama ambavyo uongozi wa chuo ulieleza.

Jengo la Kitivo cha Biashara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akizungumza leo Januari 27, 2020, na EATV & EA Radio Digital, Mussa amesema kuwa hata barua zao za kusimamishwa masomo walizopewa na uongozi wa chuo, hazikuwekwa ukomo wala tarehe ya wao kurejea chuoni ili kuendelea na masomo yao.

"Kwakweli sisi wenyewe hatufahamu kinachoendelea kwa sababu bado hatujapata taarifa ya kuitwa kwenye kikao cha nidhamu wala chuo, labda wa kulisemea vizuri waulizeni Menejimenti ya chuo, ila kwa upande wetu sisi bado tunaendelea kusubiri" amesema Rais wa DARUSO.

Desemba 18, 2019, viongozi sita wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walisimamishwa masomo yao na kuambiwa hatima yao itajulikana wakiitwa kwenye kikao cha nidhamu, kufuatia agizo la Waziri wa Elimu, Joyce Ndalichako, kutoa masaa 24 kwa uongozi wa chuo kuwachukulia hatua viongozi hao, baada ya kutoa tamko la saa 72 kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), wakiishinikiza kulipwa madai yao.