Wednesday , 29th Jan , 2020

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema kuwa Serikali imebainisha maeneo hatarishi zaidi kukumbwa na maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mafua ya virusi vya Corona kuwa ni viwanja vya ndege vya Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), Kilimanjaro, Mwanza na Bandari ya Dar es Salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Hayo ameyabainisha leo Januari 29, 2020, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari, ambapo amesema kuwa licha ya hivyo lakini hadi sasa hakuna taarifa za Mtanzania yeyote aliyekumbwa na ugonjwa huo na kutoa tahadhari kwa Watanzania watakaosafiri kwenda katika nchi ambazo zimeathirika na ugonjwa huo.

"Wizara inashauri kusubiri na kuepuka safari zisizo za lazima kwenda kwenye maeneo yaliyoathirika na inapolazimu kusafiri, basi wapate maelezo ya kitaalamu kabla ya kuondoka nchini" amesema Waziri Ummy.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, imekwishachukua hatua mbalimbali ikiwemo kuendelea kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo, kwenye mipaka yote na vituo vyote vya huduma.