Wednesday , 29th Jan , 2020

Uongozi wa klabu ya Yanga umeibuka na sakata la tuhuma za upangaji matokeo zilizoibuliwa na mlinda mlango, Ramadhani Kabwili alipokuwa akihojiwa na kipindi cha Kipenga Xtra cha East Africa Radio.

Ramadhani Kabwili

Katika mahijiano hayo yaliyofanyika Jumatatu, Januari 27, Kabwili alisema kuwa alishawishiwa na moja ya kiongozi wa klabu ya Simba kuwa atafute kadi ya njano katika mchezo mmoja kabla ya mchezo wa watani ili atimize kadi tatu na akose mchezo huo unaofuata, akimuahidi kumpa gari mpya aina ya IST.

Baada ya kauli hiyo, Shrikisho la Soka Tanzania TFF lilitoa taarifa ya kufuatilia suala hilo sambamba na klabu ya Simba, ambapo hii leo klabu ya Yanga imeibuka na kumkingia kifua mchezaji wao.

Akizungumzia tulio hilo, Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa wao kama klabu walilamikia tukio hilo mnamo Februari 12, 2019  na kocha Mwinyi Zahera, na kwamba alichokifanya Kabwili ni kuelezea historia ya tukio lenyewe lilivyokuwa.

"Kilichofanywa hapa na Kabwili ni kuelezea historia ya tukio hilo kwa uzoefu wake kwenye kucheza mechi kubwa kama ile na umri wake ni mdogo pamoja na changamoto ambazo alikutana nazo", amesema Bumbuli.

"Kwahiyo kwa sababu suala limekuwa hivyo na sisi tumemuita mchezaji wetu tukae naye na atueleze kinagaubaga nini kimetokea, tukusanye ushahidi wote na tuupeleke kwenye vyombo vinavyohusika", ameongeza.

Mtazamo wa wengi unatofautiana kuhusu suala hilo, wapo wanaosema kuwa Kabwili amekosea kulisema suala hilo katika chombo cha habari na badala yake angelipeleka TFF tena mapema zaidi na wapo wanaosema yupo sahihi kwa kuwa masuala nyeti kama hayo hayapaswi kufumbiwa macho katika soka.