Saturday , 1st Feb , 2020

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mh Jokate Mwegelo, amesema baada ya kupokea msaada wa vifaa tiba kwaajili ya watoto Njiti kutoka Doris Molllel Foundation, tayari wameshatenga jengo maalum kwaajili ya kuanza kutoa huduma hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mh Jokate Mwegelo

Akiongea leo wakati wa upokeaji wa vifaa hivyo ambavyo vitafanya huduma hiyo ianze kutolewa kwa mara ya kwanza wilayani humo, Jokate ameeleza uwepo mkubwa wa tatizo hilo hivyo msaada huo utasaidia kuwanusuru watoto hao.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa wilaya ya Kisarawe Dk. Stanford John amesema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017 hadi 2019 zaidi ya watoto 700 walizaliwa kabla ya wakati (Njiti), huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni mimba katika umri mdogo.

Aidha akikabidhi vifaa tiba hivyo vyenye thamani ya shilingi million 20 kwa mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Mkurugenzi wa Doris Molllel Foundation, amesema sababu ya kutoa msaada huo ni kutambua haki ya kuishi aliyonayo mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati kwani hata yeye ni miongoni mwa watoto waliozaliwa katika hali hiyo.

'Hii ni kuunga mkoni juhudi za Rais Magufuli na serikali kwa ujumla katika uboreshaji wa sekta ya afya nchini, amesema Doris.