Wednesday , 6th May , 2020

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda, ametoa Saa 24 kwa Wabunge wote waliokimbia kushiriki vikao vya Bunge na kwenda Dar es salaam kula bata kuhakikisha wanarudi Bungeni, tofauti na hapo watakamatwa kwa kosa la uzururaji kama wanavyokamatwa machangudoa wanaozurura usiku.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Makonda amesema kuwa Mbunge anayepaswa kuwa Dar es salaam ni yule mwenye kibali au ruhusa ya Spika wa Bunge, tofauti na hapo ni vyema wakafunga virago vyao na kurudi Bungeni ili kuepuka kukamatwa.

"Mbunge anayepaswa kuwepo ni yule mwenye kibali cha Spika, kipindi hiki ni hatari na tunataka watu wanaotoka majumbani ni wale wanaoenda kufanya kazi, hatujaalika wazururaji kutoka mikoani, inawezekana wakahatarisha zaidi maisha ya wakazi wa Dar es Salaam kwa kuwaambukiza Corona, kipindi hiki ni muhimu katika Bunge la Bajeti dhidi ya mahitaji ya wananchi" amesema Makonda.

Hata hivyo Makonda amesema kinachomshangaza ni kuona Wabunge hao wamekimbilia Dar es salaam kufurahia maisha, badala ya kwenda majimboni mwao kutembelea wananchi wanaokabiliwa na mafuriko.