Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Pia, Waziri Mkuu ametoa muda wa siku 21 kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Wizara ya Madini na wawe wameanza kutoa huduma katika eneo la Ikola ili kuhudumia wageni wanaotoka Congo.
Alitoa agizo hilo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Bandari ya Karema inayojengwa kwenye ziwa Tanganyika katika kata ya Karema wilayani Tanganyika, Katavi. Alisema mkandarasi anatakiwa ahakikishe mradi huo unakamilika haraka.
“Tumeamua kujenga bandari hii ambayo itawezesha meli zaidi ya moja kupakia na kushusha abiria na mizigo kwa wakati mmoja. Hii ni Serikali ya kuahidi na kutekeleza na ni Serikali ya kusikia na kutenda na ndio maana halisi ya falsafa ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu.”
Waziri Mkuu alisema mradi huo unalenga kuongeza tija katika shughuli za kibandari kwenye ukanda wa Ziwa Tanganyika ndani na nje ya nchi na kwamba utaongeza fursa za kibiashara nchini na pia utakuwa chachu ya kukuza uchumi pamoja na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.