Wednesday , 12th Aug , 2020

Uongozi wa klabu ya Yanga umemtaka Msemaji wa Azam Fc Thabit Zacharia 'Zaka Zakazi' athibitishe tuhuma alizotoa dhidi ya yao kuwa ndio walioandika barua iliyodaiwa kuandikwa na kiungo Salum Abubakar 'Sureboy' akiomba aruhusiwe kujiunga na Yanga.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli katika Studio za East Africa Radio kuzungumzia masuala mbalimbali ya Timu yao.

Mapema jana ilisambaa barua kwenye mitandao ya kijamii iliyodhaniwa kuandikwa na Sureboy akiuomba uongozi wa Azam Fc usikilize ofa ya Yanga, wamruhusu ajiunge na mabingwa hao wa kihistoria

Jioni ya jana Msemaji wa Azam Fc akaibuka na kuituhumu Yanga kuwa ndio iliyoandika barua hiyo na kuwa ilipelekwa ofisini kwao na mtu wa Yanga ambaye hata hivyo hakumtaja jina zaidi ya kusema mtu huyo ndiye aliyekuwa akipeleka ofa za Yanga kumtaka Sureboy

Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amemtaka Zaka Zakazi athibitishe tuhuma zake pamoja na kumtaja mtu huyo aliyewapelekea barua

"Kumekuwa na tabia ya wasemaji wa timu nyingine kutembelea nyota ya Yanga ili wapate umaarufu mitandao, hii tabia tunataka ikome kuanzia Sasa tutadili nao bila kusita"

"Kama Msemaji wa Azam Fc atashindwa kumtaja huyo mtu wa Yanga aliye peleka barua basi ajiandae kujibu mashitaka," alisema Bumbuli

Aidha Bumbuli amesisitiza kuwa Yanga haikuandika barua hiyo na haina sababu ya kufanya hivyo

"Hata ukiangalia barua yenyewe haina nembo wala jina la mtu yoyote wa Yanga"