Tuesday , 13th Oct , 2020

Kamishna Msaidizi wa Mawasiliano wa TANAPA, Paschal Shelutete, amesema kuwa moto ulioteketeza na unaoendelea kuteketeza sehemu ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, ulitokea baada ya nyasi kavu kushika moto kwa bahati mbaya wakati wa zoezi la kupasha chakula cha wageni katika kituo cha Whoma.

Kamishna Msaidizi wa Mawasiliano wa TANAPA, Paschal Shelutete, akionesha sehemu ya hifadhi za Mlima Kilimanjaro zilizoungua.

Shelutete amesema kuwa mpaka sasa serikali kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya usalama na wananchi, wameweza kufanikiwa kudhibiti moto huo lakini changamoto kubwa ni upepo mkali unaovuma nyakati za usiku unaosababisha moto kuendelea kuwaka katika maeneo mengine.

Kamishna Shelutete amewaondoa hofu Watanzania na wageni wanaotalii Mlima Kilimanjaro, kuwa eneo lililowaka moto siyo msitu bali ni eneo lenye vichaka vidogo ambalo lipo umbali mrefu kufika katika kilele cha Uhuru cha Mlima Kilimanjaro.

Moto huo ulizuka siku ya Jumapili ya Oktoba 11 mwaka huu, katika maeneo ya Mandara na Horombo na mpaka sasa juhudi za kuendelea kuuzima moto huo zinafanyika.