Monday , 2nd Nov , 2020

Klabu ya Simba imetajwa kuwa bado ni bora kuliko timu zote katika ligi kuu ya Tanzania bara msimu huu licha ya kuwa na matokeo yasiyo na muendelezo wa matokeo ya ushindi.

Aliyekuwa Kocha msaidizi wa Simba, Denis Kitambi enzi zake akiwa anafundisha kikosi cha mabingwa watetezi wa VPL.

Kauli hiyo imetolewa na aliyekuwa kocha msaidizi wa klabu hiyo, Denis Kitambi ambaye alikuwepo kwenye benchi la ufundi la Simba ambayo ilicheza robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika misimu miwili iliyopita.

''Kwakweli licha ya kupata matokeo mchanganyiko msimu huu lakini hakuna kikosi kinachoifikia Simba kwa ubora hapa Tanzania, wamekaa na wachezaji kwa muda mrefu na wanacheza mpira wa kuvutia hivyo bado wana nafasi  ya kufanya lolote msimu huu'' alisema Kitambi.

Kitambi ambaye aliwahi kuifundisha Azam kama kocha msaidizi wa Stewart Hall, alifanya kazi nchini Kenya kabla ta kurejea nchini Tanzania kuifundisha Simba.

Simba kwa sasa inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kuu ikiwa na alama 16 baada ya mechi 8 huku ikiwa imefungwa michezo miwili na sare mmoja.