Wednesday , 11th Nov , 2020

Kocha wa timu ya Tanzania, Taifa Stars, Ettiene Ndairagije ametanabaisha kwamba kambi ya nchini Uturuki ilikuwa ya mafanikio na matayarisho kwa ujumla kuelekea mchezo wao wa Novemba 13 dhidi ya Tunisia yamekamilika.

Etienne Ndairagije(Kulia) akiwa na msaidizi wake Seleman Matola(Kushoto) wakiwa wanateta jambo mazoezini.

Ndayiragije amesema wamepokea kwa masikitiko kuhusu majeraha ya nahodha wa kikosi hicho Mbwana Samatta lakini timu inabidi iendeleze ilichokianza, pia ingawa hatocheza ila uwepo wake ni muhimu katika mafanikio ya kikosi

"Tumejiandaa kwa kila hali ya kukabiliana na changamoto ikizingatiwa kuna taarifa nzuri kuwa nahodha wa ndani John Raphael Bocco amerejea katika kikosi hivyo naamini uwepo wake utaweza kuziba pengo la nahodha mkuu kwahiyo tutegemee mazuri" amesema Ndayiragije

Hata hivyo, Kocha Ndayiragije amesema taarifa kuhusu mchezaji wa kikosi hicho Adam Adam ambaye anaaminika kuwa mrithi wa nahodha Samatta kutokana na namna ya uchezaji wao na nafasi anayocheza amekosa kusafiri na kikosi kutokana na changamoto ya upatikanaji wa hati ya kusafiria hivyo amebaki nchini akisubiri kuungana na kikosi hicho itakaporejea nyumbani kujindaa na mchezo wa marejeano

Aidha, alfajiri ya hii leo, kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars sambamba na benchi la ufundi la timu hiyo kimeanza safari ya kutoka jijini Istanbul Uturuki, kuelekea jiji la TunisTunisia, licha ya uimara na ubora wa Tunisia Kocha Ndayiragije amesema mchezo huo ni muhimu sana kwao kuonesha kwa namna ganin wao pia wana kikosi bora.