Wednesday , 11th Nov , 2020

Klabu ya Yanga, inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya African Lyon ya ligi daraja la kwanza siku ya jumapili, mchezo huo utachezwa uwanja wa Azam Complex saa 1:00 usiku.

Yanga ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo kwenye michezo ya ligi kuu soka Tanzania bara mismu huu wa 2020-21

Yanga watautumia mchezo huo kama sehemu ya kocha Cedric Kaze kuendelea kukiweka fiti kikosi hicho cha mabingwa wa kihistoria wa Tanzania bara. Katika maandalizi kuelekea mchezo huo wa kirafiki, kikosi hicho kitaingia kambini kesho baada ya mapumziko ya siku 4.

Wachezaji 24 ndio wanaotarajiwa kuingia kambini, ambapo wachezaji 20 ni wa kikosi cha kwanza wale ambao hawajaitwa kwenye timu zao za taifa kipindi hiki ambacho ligi imesimama kwa takribani wiki mbili kupisha kalenda ya kimataifa ya FIFA. Wachezaji wanne mwalimu Kaze atawaita kutoka timu ya vijana.

Africa Lyon ambayo inafundishwa na nahodha wa zamani wa klabu ya Yanga Nizar Khalfan, imeshinda mchezo mmoja tu kati ya michezo minne, iliyocheza kwenye michezo ya kundi A ya ligi daraja la kwanza, wamefungwa michezo miwili na wametoka sare mchezo mmoja. Wapo nafasi ya 6 wakiwa na alama 4 ikiwa ni tofauti ya alama 8 dhidi ya Afrcan Sports wanaoongza kundi hilo wakiwa na alama 12.

Mpaka sasa Yanga ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo kwenye michezo ya ligi kuu soka Tanzania bara, msimu huu, wameshinda michezo 7 sare michezo 3 ukiwemo mchezo dhidi ya watani zao Simba SC. Inashika nafasi ya 2 kwenye msimamo ikiwa na alama 24.