Thursday , 3rd Dec , 2020

Mwenyekiti wa Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, ameiomba serikali kuendeleza juhudi za makusudi katika kuhakikisha watu wenye ulemavu, wanawekewa mazingira mazuri ya kupata mahitaji yao kulingana na hali zinazowakabili.

Mwenyekiti wa Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Desemba 3, 2020, wakati wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu, pamoja na pongezi hizo kwa serikali, Tume inatambua juu ya kuwepo watu wenye ulemavu unaoonekana na usioonekana.

Aidha, Tume imewawataka wananchi wanaoishi na watu wenye ulemavu kuchukua hatua za kuwasaidia na kuwaona kuwa  sehemu yao. 

Mbali na hayo Tume hiyo pia, imewataka wananchi kuachana na imani, mila, desturi na mitazamo potofu ambayo huwafanya watu wenye ulemavu kuvunjika moyo na kujiona hawakubaliki, hawawezi na hawana mchango wowote kwa jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla katika shughuli zinazohusu maendeleo.