Thursday , 24th Dec , 2020

Klabu ya PSG imemfuta kazi kocha Thomas Tuchel, ikiwa ni masaa machache baada ya kukiongoza kikosi hicho kuibuka na ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Strasbourg na kocha wa zamani wa Tottenham, Mauricio Pochettino anatajwa kama mbadala wake.

Kocha Thomas Tuchel

Mkurugenzi wa Michezo wa PSG Leonardo amemfuta kazi kocha huyo mjerumani mwenye umri wa miaka 47, licha ya kikosi hicho kupata ushindi mkubwa usiku wa jana kwenye mchezo wa ligi kuu French Ligue 1.

Lakini pia ikiwa ni miezi 4 tu tangu alipokiongoza kikosi hicho, kwenye fainali ya klabu Bingwa barani Ulaya, mchezo ambao walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Bayern Munich.

Tuchel amekuwa akikosolewa juu ya mwenendo wa kikosi hicho, ambao umekuwa sio wa kuridhisha, ingawa kocha huyo pia alinukuliwa akionyesha kutoridhishwa na jinsi mambo yanavyoendeshwa ndani ya klabu hiyo, huku akisema anahisi kama yupo kwenye klabu ya siasa.

PSG wapo nafasi ya 3 kwenye msimamo wa ligi kuu Ufaransa Ligue 1, wakiwa na alama 35, tofauti ya alama 1 na vinara Lyon na Lille walio nafasi ya pili, wakiwa na alama 36. Lakini pia timu hiyo imefuzu hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo watacheza dhidi ya Barcelona kwenye hatua hiyo.

Thomas Tuchel alijiunga na PSG Mei 14 mwaka 2018, akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani, ambapo amekiongoza kikosi hicho cha matajiri wa jiji la Paris kwenye michezo 127, ameshinda michezo 95, sare michezo 13 na kafungwa michezo 19. Huku akishinda jumla ya mataji 6.

Kwa sasa inaripotiwa kuwa PSG wapo kwenye mazungumza na kocha wa zamani wa Tottenham Mauricio Pochettino, ambaye kwa sasa hana timu.