Friday , 25th Dec , 2020

Kocha wa Singida United Edwin Agayi amesema hali mbaya ya kiuchumi ndio sababu iliyopelekea timu hiyo kushushwa daraja, timu hiyo imeshushwa madaraja mawili baada ya kushindwa kufika uwanjani, kwenye mchezo wa ligi daraja la kwanza dhidi ya Alliance.

Michezo yote ya Singida United waliokuwa wamecheza imefutwa na wameshushwa madaraja mawili

Kamati ya uendeshaji na usimamizi wa Ligi Tanzania bara TPLB katika kikao chake cha Disemba 22, 2020, kilifanya maamuzi ya kuishusha madaraja mawili klabu ya Singida United, sambamba na matokeo yake ya michezo yote kufutwa kwa kosa la kushindwa kutokea uwanjani katika mchezo wa ligi daraja la kwanza dhidi ya Alliance FC.

Kocha wa kikosi hicho Edwin Agayi amesema sababu kubwa hasa iliyosababisha timu hiyo kufikia katika hali hiyo ni kutokana na timu kuwa na hali mbaya ya kiuchumi.

“Kwakweli changamoto kubwa ilikuwa ni hali ya kiuchumi haya mengine yote yametokea lakini tatizo kubwa ni hali ya kiuchumi, ambalo lilisababisha kuna wakati timu kushindwa kusafiri, kuna wakati wachezaji wakawa wanagoma kwenda kucheza kwa sababu kuna kiti walikuwa wanadai hiyo sababu kubwa ilikuwa ni hiyo”, amesema.

Kocha Agayi alipoulizwa kuhusu nafasi ya viongozi na ukaribu wao na timu alisema kuwa timu ilikuwa haipati huduma nzuri kama hapo awali na yeye alikuwa hajui ni kwa nini, akasisitiza kuwa ilikuwa ni ngumu hata kwa watu wa pembeni kuisaidia timu kwa sababu Singida United ni kampuni hivyo mtu kutoka nje ingekuwa ngumu kuisaidia timu.

Kuhusu nafasi na mchango wa Rais wa heshima wa klabu hiyo Mh. Mwigulu Nchemba ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria na Mkurugenzi wa klabu hiyo Festo Sanga ambaye kwa sasa ni mbunge wa jimbo la Makete, kocha Agayi alisema,

''Najua hii timu ni ya watu wawili, hawa kina Festo ni waajiriwa wenzangu kwa hiyo haya yalipoanza kutokea tulikuwa tunaulizana, ukimuuliza katibu naye anakwambia nafatilia, lakini kadri siku zinavyoenda hali inakuwa mbaya”.

Michezo yote ya Singida United waliokuwa wamecheza imefutwa na wameshushwa mpaka ligi ngazi ya wilaya.