Junior Lokosa anajiunga na Simba akiwa mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba na klabu ya Esperance ya Tunisia mwezi Julai mwaka 2020
Lokosa mwenye umri wa miaka 27 anajiunga na Simba akiwa mchezaji huru mara baada ya kuvunja mkataba na klabu ya Esperance ya Tunisia mwezi Julai mwaka 2020. Huu unakuwa ni usajili wa 3 kwa klabu ya Simba katika dirisha hili dogo la usajili, baada ya kuwasajili viungo Perfect Chikwende kutoka FC Platnum ya Zimbabwe na Taddeo Lwanga raia wa Uganda.
Usajili wa Lokosa anakamilisha idadi ya washambuliaji 4 kwenye kikosi cha mabingwa wa Tanzania bara, anaungana na John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu.
Kwa sasa kikosi cha Simba kinanolewa na kocha mfaransa Didier Gomes Da Rosa, ambaye alitambulishwa hapo jana akichukua mikoba ya kocha Sven Vandenbroeck aliyetimkia AS FAR ya Morocco, Simba inafanya usajili huu ikiwa ni katika harakati za kuhakikisha wanafanya vyema kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika ambapo wamejiwekea malengo ya kufika hatua ya nusu fainali msimu huu.
Simba imepangwa kundi A’ Sambamba na mabingwa wakihistoria na watetezi Al Ahly ya Misri, AS Vital Club ya Congo na AL Merrikh ya Sudani.