Thursday , 28th Jan , 2021

Mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu nchini England, klabu ya Manchester United imeshindwa kukwea kileleni kwenye msimamo wa ligi kuu nchini humo baada ya kipigo cha mabao 2-1 usiku wa kuamkia leo tarehe 28 Januari 2021 kutoka kwa klabu ya Sheffield United inayoshika mkia.

Baadhi ya wachezaji wa Manchester United wakionekana kuhuzunika baada ya kufungwa bao la pili dhidi ya Sheffield United usiku wa kuamkia jana.

Sheffield ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao, lililofungwa na mlinzi wake wa kushoto Kean Bryan dakika 23 ya mchezo na Manchester United wakajiuliza na kusawazisha kupitia kwa nahodha wake, Harry Maguire aliyefunga bao dakika ya 64 kwa kichwa baada ya kona ya Alex Telles.

Licha ya wenyeji hao wa Old Trafford kuonekana kuutawala mchezo kwa kuwa na ulimiki mkubwa wa mpira, lakini walikuwa ni Sheffield United waliofanikiwa kuibuka na ushindi  kwa kufunga bao la pili lililofungwa na Oliver Burke dakika ya sabini ikiwa ni dakika tano tu tokea aingie akitokea benchi.

Kipigo hicho kimewafanya Manchester United kushindwa kukwea kileleni mwa EPL na kusalia nafasi ya pili wakiwa na alama 40 na kuwakabidhi usukani watani wao wa jadi klabu ya Manchester City ambayo hivi sasa ipo kileleni ikiwa na alama 41 tena mchezo mmoja nyuma ya Manchester United.

Ushindi huo wa Sheffield chini ya kocha wake Chris Wilder ni wa pili tokea msimu huu uanze na wanaendelea kushika mkia lakini wameweka rekodi ya kufunga mabao mawili mara mbili kwenye mchezo mmoja msimu huu tena michezo yote miwili ikiwa dhidi ya Manchester United.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza, Sheffield walifungwa mabao 3-2 na Manchester United, lakini mchezo wa usiku wa jana waliweza kulipa kisasi kwa kushinda kwa mabao 2-1 ilhali kwenye michezo yake mingine ikiwa haijawahi kufunga bao zaidi ya moja kwenye EPL msimu huu.

Manchester United wameweka rekodi ya kufungwa mara nne kwenye dimba lake la nyumbani 'Old Trafford' msimu huu katika michezo 10 waliyocheza kwenye EPL pekee ikiwa ni vipigo vingi zaidi katika msimu mmoja wa EPL.