Friday , 29th Jan , 2021

Mzazi mmoja mkazi wa kijiji cha Ilanga, kata ya Mlale, iliyopo wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe, amegoma kumpeleka mwanaye kujiunga na kidato cha kwanza akidai kuwa mwanaye hana akili na kwamba watoto wamekuwa wakichapwa tu wanapokuwa shuleni.

Anania Mdolo, Mzazi ambaye hajapeleka mwanaye shule

Mzazi huyo anayejulikana kwa jina la Anania Mdolo, ameyabainisha hayo wakati wa ziara ya mkuu wa wilaya ya Ileje, Joseph Mkude, akiwa katika operesheni ya kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanaripoti shuleni na ndipo alipobaini uwepo wa mtoto Happy Mdolo, aliyetakiwa kuripoti shule ya sekondari Mlele, akigomewa kuendelea na masomo na baba yake mzazi.

Awali akizungumza na kueleza sababu ya kuacha kumpeleka mwanaye shule, Mzee Mdolo, alidai kuwa sababu kubwa ni kwamba mwanaye hana akili za kuendelea na masomo.

"Nina watoto 9, Happy haaenda kujiunga na kidato cha kwanza niliona akili yake haifai kuendelea na masomo, alama zake ni ndogo alipata wastani wa C, shuleni watoto ni kuchapwa viboko tu kila siku wakati hana akili, akianza kuchapwa viboko kila siku mtanisaidiaje?", amesema mzazi huyo.

Licha ya vuta ni kuvute kati ya mkuu wa wilaya na mzazi huyo, hatimaye mkuu huyo wa wilaya akampa fomu ya maelekezo na mahitaji yote ya mtoto, huku akimtaka mzazi huyo kumpeleka mtoto shule mara moja.