Saturday , 30th Jan , 2021

Washika mitutu wa jiji la London, klabu ya Arsenal watashuka dimbani usiku wa leo tarehe 30 Januari 2021 kukipiga na wapinzani wake wa muda mrefu klabu ya Manchester United mishale ya saa 2:30 usiku kwenye ligi kuu nchini England.

Mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford akijaribu kuwatoka walinzi wa Arsenal kwenye mchezo wa awali walipokutana EPL 2020.

Mchezo huo unamfanya kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjear kuwa na kibarua kizito cha kufuta unyonge mbele ya wapinzani wake hao baada ya kucheza michezo minne bila kupata ushindi, akifungwa 3 na kupata sare 1.

Rekodi hiyo inamfanya Solskjear kuwa kocha wa kwanza kwenye historia ya Mashetani wekundu hao kucheza michezo mingi, minne dhidi ya Arsenal na kushindwa kupata ushindi.

Arsenal ambayo ipo nafasi ya 9 wakiwa na alama 30, alama 10 nyuma ya United, hawana uhakika kama nahodha wake Pierre Emerik Aubameyang atakuwepo baada ya nyota kuripotiwa kumuuguza mama yake mzazi.

Licha ya nahodha huyo kuwa mashakani kwenye mchezo huo, lakini Pablo Mari, Kieran Tierney, Emile Smith Rowe na Daniel Ceballos wamerejea kikosini baada ya kupona majeraha yao na usajili mpya Martin Odegaard ukijumuishwa kikosini.

Kwa Upande wa Manchester United, wanatazamiwa kuwa na mlinzi wake Erick Bailly na Anthony Martial ambao walikuwa na majeraha madogo hata kumfanya Bailly kuukosa mchezo uliopita dhidi ya Sheffield United waliofungwa 2-1.

Rekodi za michezo mitano ya mwisho wawili hao walipokutana kwenye EPL, Manchester United imeambulia ushindi 1 tu na kutoka sare 1 na kukubali kupoteza michezo mitatu.

Kwa upande wa rekodi za jumla, Manchester United bado inaongoza kwa kumfunga zaidi Arsenal, kwenye michezo 56 ya EPL pekee, Manchester United imepata ushindi michezo 24, sare 17 ilhali Arsenal akishinda michezo 16.

Michezo mingine ya EPL itakayochezwa leo  ni, Everton dhidi ya Newcastle United saa 9:30 alasiri, Crystal Palace dhidi ya Wolves, Manchester City dhidi ya Sheffield United, West Bromwich dhidi ya Fulham zote tatu kuchezwa saa 12:00 jioni, SOTON na Aston Villa wakicheza saa 5:00 usiku.