Thursday , 11th Mar , 2021

Michuano ya UEFA Europa ligi inataraji kuendelea usiku wa leo kwa michezo nane ya mtoano hatua ya 16 bora huku Manchester United na Arsenal zote za England zikitaraji kuwakosa nyota wake kadhaa kutokana na wachezaji hao kupata majeraha.

Kombe la michuano ya UEFA EUROPA ligi la msimu huu wa mwaka 2020-2021.

Kwa upande wa Manchester United ambao watashuka dimbani saa 2:55 usiku wa leo Machi 11 kukipiga na AC Milan ya Italia, huenda ikamkosa mshambuliaji wake Marcus Rashford mwenye maumivu ya kifundo cha mguu alichoyapata wikiendi iliyopita dhidi ya Manchester City.

Mshambuliaji mwengine atakaye kosekana ni Edinson Cavani mwenye maumivu ya nyama za paja, mlinda mlango David De Gea mwenye matatizo ya kifamilia, viungo Donny Van De Beek na Juan Mata wenye maumivu ya mguu.

Klabu ya AC Milan ambao ndiyo wageni wa mchezo huo, na wao wamethibtisha kuwa watawakosa nyota wake 6 wa kikosi cha kwanza wenye majeraha,mfungaji wake tegemezi wa sasa, mkongwe Zlatana Ibrahimovic, Mario Mandzukic, viungo: Hakan Calhanoglu na Ismail Bennacer.

Wengine ni mlinzi wa kushotoTheo Hernandez na mshambuliaji Ante Rebic ambao baadhi yao wanatazamiwa huenda wakarejea kwenye mchezo wa marejeano juma lijalo.

Mara ya mwisho Manchester United kukutana na AC Milan kwenye michuano ya ushindani barani ulaya ni mwaka 2010 ambapo Manchester United waliitoa Milan kwenye 16 bora kwa kuwafunga jumla ya mabao 7-2 kwenye michezo miwili baada ya kupata ushinda wa mabao 4-0 na kufungwa 3-2.

Kwenye rekodi za jumla, Wawili hao wamekutana mara 8, kila mmoja akishinda mara 3 na kutoa sare 1.

Kwa upande wa 'Washika mitutu wa jiji la London' klabu ya Arsenal, wamethibitisha kuwa kiungo wake mshambuliaji Emile Smith Rowe ana majeraha ya mguu hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuukosa mchezo dhidi ya Olympiacos ya Ugiriki utakaochezwa saa 5:00 usiku wa leo.

Michezo mingine ya UEFA EUROPA ligi itakayochezwa saa 2:55 usiku wa leo ni: 

Ajax ya Uholanzi dhidi ya Young Boys ya Uswizi, Nyambizi wa nchini Hispania klabu ya Villareal itakuwa wageni wa Dynamo Kyiv ya Ukraine wakati huo huo Slavia Prague ya Jamhuri ya Czech itachuana na Rangers ya nchini Scotland.

Molde ya Norway wamesafiri kuifuata Granada ya Hispania, AS Roma ya Italia itakuwa wenyeji wa Shakhtar Doneskt ya nchini Ukraine ilhali Tottenham Hotspurs itakipiga na Dynamo Zagreb ya nchini Croatia, michezo mitatu hii kuchezwa saa 5:00 usiku wa leo.