
Profesa Athuman Kapuya
Akizungumza na kipindi cha Kipenga cha East Africa Radio, Profesa Kapuya ambaye pia ni mjumbe wa baraza la wadhamini wa Simba alisema, ''hali ya uchumi wa klabu inawapa uhakika wa maisha wachezaji, usajili wenye tija kwa idara husika za timu, na eneo la utaalamu, katika maeneo yote yanaohitaji utaalamu na mwisho ubora wa benchi la ufundi linachagiza mafanikio haya.''
Akifafanua zaidi amesema, ''mchezaji anayeichezea Simba kwa sasa anauhakika na maisha kutokana na maslahi bora anayoyapata ndani ya timu, posho na bonasi mbalimbali kadri walivyokubaliana, mshahara kuingia kwa wakati matibabu bora katika hospitali za ndani na nje ya nchi kwa wachezaji pindi wanapopata majeraha.''
Ameeleza kuwa viwango vya wachezaji pia vipo bora kwa mchezaji mmoja mmoja na timu kiujumla akiwa na maana ya usajili ulizingatia mahitaji sahihi kwa eneo sahihi kwa mfano wa mchezaji kama Luis Miquissone, Chama , Bwalya, Lwanga na Onyango.
Pia amesema Simba imezingatia kuajiri wataalamu katika maeneo yote yanayohitaji wana taaluma tofauti tofauti kama vile eneo la saikoloji za wachezaji, wamemuajiri gwiji wa mambo hayo, mtathimini viwango 'video analyst' pia wana benchi la ufundi lililoshehena wabobezi likiwa chini ya Didier Gomez Da Rosa mwenye uzoefu na soka la Afrika katika ngazi ya vilabu.
Kapuya aliyekuwa na furaha kubwa mara baada ya timu yake kuwafunga El Merrikh ya Sudan mabao 3-0 kwenye uwanja wa Mkapa, alisita kusema kama timu yake wanaweza kutwaa ubingwa zaidi ya kusema atawafuatilia zaidi wapinzani wao.
Timu ya Simba ambayo ni ya pili katika msimamo wa ligi kuu ikiwa na point 46 nyuma ya vinara katika msimamo Yanga Africa wenye pointi 50 wakiwa mbele kwa michezo 3, huku wakifanya vyema katika mashindano ya kimataifa wakiwa wamecheza michezo 4 wanapoint 10 wanaongoza kundi A lenye timu za Al Ahly , El Marrikh na As Vita.