Sunday , 11th Apr , 2021

Klabu ya soka ya Real Madrid imejiweka pazuri kwenye mbio za kusaka taji la Ligi kuu nchini Hispania baada ya usiku wa Aprili 10, 2021 kuwafunga wapinzani wao Barcelona magoli 2-1 kwenye mchezo uliopigwa Santiago Bernabeu.

Lionel Messi na Karim Benzema

Baada ya mchezo huo ambapo magoli ya Real Madrid yalifungwa na Karim Benzema pamoja na Toni Kroos huku lile la Barcelona likifungwa na Oscar Mingueza, rekodi mbalimbali ziliwekwa.

Miaka 13 imepita tangu Real Madrid iifunge Barcelona kwenye michezo miwili ya La Liga, nyumbani na ugenini ndani ya msimu mmoja. Msimu huu katika mchezo wa kwanza Real Madrid ilishinda ugenini magoli 3-1.

Lionel Messi hajafunga goli kwenye El Clasico 7 mfululizo ambapo mara ya hivyo kufunga ilikuwa msimu wa 2017-2018 Kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya 2-2 pale Camp Nou.

Baada ya ushindi huo, Real Madrid wamekwea kileleni mwa msimamo wa La Liga wakiwa na alama 66, sawa na Atletico Madrid wanaoshika nafasi ya pili lakini Atletico ana mechi moja pungufu. Barcelona ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 65 hivyo kufanya mbio za Ubingwa wa La Liga kuendelea kuwa kitendawili.