Thursday , 15th Apr , 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Ummy Mwalimu amesema moja ya jambo lililowachelewesha kuleta muswada wa bima ya afya ni suala la kuunganisha huduma za wazee na bima ya afya.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Ummy Mwalimu

Mh. Ummy amesema hayo leo bungeni wakati akijibu swali la nyongeza liloulizwa na Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini Dk. Oscar Ishengoma Kikoyo liliosema; "Pamoja na nia njema ya serikali kutoa matibabu bure kwa wazee wetu zoezi zima limegubikwa na ukiritimba, Je, serikali haino busara kuainisha vitambulisho vinavyotolewa kwa wazee na bima ya afya ili wazee wetu wapate tiba stahiki?”.

Akijibu swali hilo Mh. Ummy amesema "Suala la kuunganisha huduma za wazee na bima ya afya ni jambo moja lililotucheleshwa kuleta muswada wa bima ya afya kwenye bunge lako ilikuwa kuweka utaratibu kama huo, pale ambapo serikali italeta muswada wa bima ya afya itaweka utaratibu ambao utaondoa hizi changamoto za matibabu bure kwa wazee”.

Ameongeza kuwa, Ofisi ya Rais TAMISEMI inatekeleza Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003, kwa kufanya utambuzi wa Wazee na kuwapatia huduma mbalimbali za Afya katika Mikoa mingine inaendelea kufanya utambuzi kwa wazee na kuhakikisha wazee wote waliotambuliwa wanapewa vitambulisho vya matibabu bure.