Monday , 19th Apr , 2021

Kwa mujibu wa tovuti ya Sky Sports ya nchini England, kocha Jose Mourinho amefukuzwa kazi na klabu ya Tottenham Hotspurs kufuatia mwenendo wa matokeo yasiyoridhisha klabu hapo hususani kwenye ungwe ya pili ya ligi kuu nchini England.

Aliyekuwa kocha wa Spurs, Jose Mourinho.

Mourinho ambaye alijiunga na Spurs Novemba 20, 2019 kuchukua mikoba ya Mauriccio Pochettino na kusaini kandarasi hadi mwaka 2023, aliiongoza Spurs jumla ya michezo 86 kwenye michuano yote huku akipata ushindi kwenye michezo 44, sare 19 na vipigo 23.

Mourinho ameiacha Spurs kwenye nafasi ya saba kwenye msimamo wa EPL wakiwa nyuma kwa alama 5 kuingia kwenye nafasi nne za juu ili kuwani atiketi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa msimu ujao wa mwaka 2021-2022.

Licha ya Mourinho kuiongoza Spurs kutinga fainali ya kombe la Carabao litakalochezwa tarehe 25 Aprili 2021 dhidi ya Manchester City, lakini mashabiki wa Spurs walishuhudia wakitolewa kwa kipigo cha mabao 5-4 dhidi ya Everton na kutolewa kwenye kombe la FA.

Kwa upande mwingine, Spurs iliondoshwa kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya ligi ya Europa kwa kipigo cha kupinduliwa meza cha mabao 3-0 baada ya kushinda 2-0 mchezo wa kwanza dhidi ya Dynamo Zagreb majuma mawili yaliyopita na kuushtua Uongozi wa Spurs.

Hii ni mara ya nne Mourinho kutimuliwa kazi kufuatia mwenendo wa matokeo yasioridhisha kwani mwaka 2007 mwishoni alitimuliwa na Chelsea, 2012 alitimuliwa na Real Madrid, miaka miwili mitatu mbele akatimuliwa na Chelsea na mwaka 2018 Disemba alitimuliwa na Man Utd.