Monday , 26th Apr , 2021

Klabu ya soka ya Simba itamkosa kiungo wake mahiri Thaddeo Lwanga  kwenye mechi ya kesho Ligi  Kuu ya Tanzania bara dhidi ya Dodoma Jiji kutokana na kuendelea kuwa nchini mwao Uganda baada ya kufiwa na dada yake wiki iliyopita.

Kiungo mkabaji wa Simba, Taddeo Lwanga akiwania mpira wa mlinzi wa AS Vita, Ebunga kwenye mchezo wa klabu Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari kocha msaidizi wa klabu hiyo,Seleman matola amesema kukosena kwa Lwanga sio sababu ya wao kushindwa kupata matokeo na wamejiandaa vizuri kuikabili Dodoma jiji kwa lengo la kuendeleza mbio za kuwania ubingwa.

Katika hatua nyingine, Matola amesema wachezaji Luis Miquissone na Pascal wawa ambao walikosekana kwenye mchezo dhidi ya Gwambina Fc kutokana na kutumikia adhabu ya kadi wamerejea kikosini.

“Luis Miquissone na  Pascal Wawa wamemaliza adhabu zao za kadi tatu za njano ambazo walipata hivyo watakuwa katika sehemu ya mchezo kesho endapo kocha mkuu Didier Gomes ataamua kuwatumia ”Kocha msaidizi Seleman Matola.

Katika mchezo wa duru la kwanza VPL, timu hizo zilipokutana kwenye uwanja wa  Jamhuri ,Dodoma Jiji ilikubali kichapo  cha bao 1 – 2 , hivyo  mchezo wa kesho unatarajiwa kuwa ni wa kisasi . 

Simba  inaongoza  ligi ikiwa na alama 58 baada ya mechi 24  inakutana na Dodoma jiji ambayo ipo nafasi  ya 7  ina pointi 38  na imecheza mechi 27.