Friday , 2nd Jul , 2021

Waganga 87 wa tiba asilia wamefanikiwa kujenga vyumba viwili vya madarasa kwa kutumia fedha zao za uganga, katika Shule ya Sekondari ya Chinameli Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, ili kuunga mkono jitihada za Serikali kuinua kiwango cha elimu wilayani humo.

Picha: Vyumba vya madarasa vilivyojengwa na waganga wa tiba asilia mkoani Simiyu.

Akizungumza na EATV, Mshauri wa waganga wa Tiba Asilia Mkoa wa Simiyu, Ndabagija Katani, amesema kazi ya maendeleo haipaswi kuachwa kwa Serikali peke yake huku akiwashauri waganga wengine nchini kuiga mfano huo.

“Sisi tulianzia kujenga kituo cha polisi, tukashirikiana sisi wataalamu wa tiba asili baadaye tukachimba visima vya shule kwa wanafunzi na tukaona tujenge madarasa mawili hapa, pesa tunazo sisi ni wafugaji wa ngombe tulikuwa tunaleta kila mmoja mifuko miwili,” amesema Bw. Katani.

Naye Mbunge wa Jimbo la Itilima Njalu Silanga amesema kitendo walichokifanya waganga hao ni cha kushangaza taifa kwani kinaonesha jinsi ngani waganga wanauelewa juu ya miradi ya maendeleo na kuwa na muamko katika kuchangia kuinua hususan elimu.

Vyumba hivyo viwili vya madarasa vilivyojengwa katika Shule ya Sekondari ya Chinameli vilivyogharimu shilingi milioni 29 vimewekewa Jiwe la Msingi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Luteni Josephine Mwambashi.