Tuesday , 6th Jul , 2021

Kikosi cha mabingwa wa Kihistoria wa Tanzania bara Yanga SC kitaingia kambini kesho Jumatano Julai 7, 2021, tayari kwa maandalizi ya michezo miwili ya Ligi kuu na ule wa fainali ya kombe la FA dhidi ya watani zao Simba SC. Kikosi hicho kinarejea baada ya mapumziko ya siku nne.

Kikosi cha Yanga SC

Kupitia kipindi cha michezo cha Kipenga kupitia East Africa Radio kinachoruka kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia Saa 2:00 mpaka Saa 3:00 Usiku, Msemaji wa klabu ya Yanga Hassan Bumbuli amethibitisha kuwa kikosi hicho kitarejea kambini hapo kesho.

“Baada ya mechi dhidi ya Simba wachezaji walipewa mapumziko ya siku nne kwa hiyo tunatarajia kikosi kitarejea siku ya Jumatano pale Avic Town kwa ajili ya kujianda na mechi mbili zilizobakia, lakini pia mechi moja ya kombe za Azam Sports Federation Cup ambayo tutakwenda kucheza kule mkoani Kigoma dhidi ya watani wetu wa jadi tena Simba. Ikiwa kwa mara ya pili ndani ya mwezi mmoja tunakutatana nao kwa hiyo wachezaji wamepumzika wanaendela kula bata, na kwa sababu kulikuwa na bonasi nzuri wamepatiwa kwa hiyo tumewapa nafasi wakajivinjali wafurahi.” Amesema Hassan Bumbuli

Wachezaji wa Yanga walipewa mapumziko haya baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa Julai 3, 2021 katika dimba la Benjamini Mkapa Dar es Salaam bao pekee la mchezo huo lilifungwa na Zawadi Mauya dakika ya 12 ya mchezo na kuifanya Yanga kutopoteza mchezo wa Ligi dhidi ya Simba kwa msimu wa pili mfululizo.

Yanga wamebakiza michezo miwili ya Ligi Kuu dhidi ya Ihefu FC mchezo huu utachezwa Julai 14 na Yanga watakuwa wenyeji, na watamaliza msimu wa Ligi Kuu kwa kucheza ugenini dhidi ya Dodoma Jiji Julai 18, kabla ya kwenda kucheza mchezo wa fainali ya Azam Sports Federation Cup dhidi ya Simba SC Julai 25 huko mkoani Kigamo katika dimba la Lake Tanganyika.