
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof.Elisante Ole Gabriel akiapaa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo, Ikulu Jijini Dar es Salaam
Akizungumza mara baada ya uapishwo wa mabalozi na mtendaji mkuu wa mahakama ya Tanzania Rais Samia amesema serikali ipo kwenye maboresho makubwa ya mahakama pamoja na majaribio ya mahakama zinazotembea ambazo zimeonekana zinafanya vizuri mkoa wa Dar es Salaam.
"Nianze na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, mengi yalishasemwa. Una kazi ya kuhakikisha magereza hayajai watu wasio na makosa kwamba haki inatendeka. Pili unapaswa kuhakikisha watumishi wanafanya kazi katika mazingira mazuri na maslahi yao," amesema Rais Samia.
Akizungumzia kuhusu uteuzi wa Prof. Elisante Gabriel kutoka kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mifugo) hadi Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania amesema, “Pengine wengi wanaweza kushangaa kwanini Maasai ametolewa kwenye ng'ombe na kupelekwa kwenye Mahakama (Mtendaji Mkuu wa Mahakama), lakini najua unaweza kufanya vizuri eneo hilo. Kwahiyo achana na ng'ombe kwa sasa nenda kawatumikie watu" amesema Rais Samia